Rais JAKAYA KIKWETE ameahidi kutoa mifuko 100 ya saruji, kwa kila familia kwa Wakazi waishio katika Mji Mpya wa Mabwepande, Jijini Dar es salaam ili kuwawezesha kujenga Makazi ya kudumu huku akiwakabidhi hati za kumiliki kihalali maeneo wakazi wapatao 604. Akizungumza mara baada ya kuzindua Kituo cha Polisi, Nyumba za Walimu, pamoja na Shule ya Msingi Mabwepande , Rais KIKWETE amesema fedha zitakazotumika kwa ajili ya ununuzi wa mifuko hiyo zitakabidhiwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni hapo kesho. Rais KIKWETE ametumia fursa hiyo kuwaomba Wahisani mbalimbali kuunga mkono Juhudi mbalimbali za kuwasaidiua Wakazi wa Mabwepande katika kuwawezesha kujenga makazi ya kudumu na kuondokana na adha wanazokumbana nazo kutokana na uchakavu wa mahema. Kwa upande wake Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es salaam, DCP SULEIMAN KOVA, ameelezea hatua zitakazochukuliwa na Jeshi la Polisi nchini katika kuimarisha zaidi ulinzi kwa Wakazi wa Mabwepande. Awali akizungumza mara baada ya kuzindua Daraja la Golani, lililoko Kimara Suka, katika Kata ya Saranga, Jijini Dar es salaam Rais KIKWETE amesema atakutana na Uongozi wa Wizara ya Maji pamoja na ule wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa lengo la kulipatia ufumbuzi tatizo la muda mrefu la maji linalowakabili baadhi ya Wakazi wa Manispaa hiyo hususani wale wanaoishi eneo la Kimara, Jijini humo
0 comments:
Post a Comment